
SUNDAY SERVICE ON 06 APRIL, 2025
Pastor NINA SEDEKIA
HOLY SPIRIT CHURCH, DAR ES SALAAM
ZABURI 1:4
Sivyo walivyo wasio haki;
Hao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.
WALE AMBAO HAWANA NAFASI YA MUNGU
Upendo wa Mungu hauchagui kabila wala rangi.
Acha wakuone huna akili. Wewe songa mbele. Wasiompenda Mungu wanaonekana kama makapi.
Wale walio na Yesu wana kitu cha kujivunia, cha kujihami nacho, cha kujitetea nacho. Wasio na Mungu ni makapi tu.
ZABURI 1:1
Heri mtu yule asiyekwenda
Katika shauri la wasio haki;
Wala hakusimama katika njia ya wakosaji;
Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.
Wasio haki vikao vyao ni vya maovu.
Je, wewe baraza lako likoje? Stori zako zikoje? Jana mmoja alikuwa nyumbani na mwingine kazini, stori zako ni zipi?
Wale wanaojua kwamba nikiongea vya watu natenda dhambi, waache mara moja. Heri haiangalii upande wa mwili wa nyama, Heri yule anayeitwa heri katika ufalme wa Mungu.
Hawa ndio wale waliochaguliwa.
Unamteta Mtu ambaye baada ya mda mfupi huyo huyo unamwomba chumvi, ni hatari. Tumwombe Mungu atupe akili na maarifa ili hiyo tabia ikome.
Ni kijana au binti umekuja kufanya kazi kwenye nyumba ya mtu, usiwe mmbeya. Fanya kazi iliyokuleta katika nyumba hiyo.
Mwingine umekuja kutembea, matembezi yako yawe salama, utembee vema.
Utakaporudi kwenu usije ukawambia wa kwenu mabaya kwa sababu ya matembezi yako yaliyo mabaya. Sema wanamuonea wivu huyu, katangaze, waambie mnamwonea wivu. Neno lako litathibitika. Heri wewe utakayekuwa balozi mwema wa Ufalme wa Mungu.
Kazini kwako na kila unapopita uonekane una heri. Usije bure ukaonekana kwamba wewe si chochote mbele za Mungu.
Anayeishi kwa Imani ni yule anayesimama kwa uhakika. Kwa sababu Imani ni kuwa na hakika.
Ni imani iliyo na subira, iliyo na ujasiri, iliyo ya kuthubutu, ya adabu, heshima, iliyo ya kweli.
Usikubali kuvalishwa fedheha kwa kutenda yaliyo ya aibu au yaliyo mabaya.
Wa Imani ni watu gani? Ni wale ambao Mungu anamwambia kwamba kila utakachotia mikono kimebarikiwa. Ni wale ambao wamedhamiria kumwona Mungu.
Mfano: Nimepanda mapapai, wakati wa jua kali nikamwagilia, yalipofikia kutoa maua, yalionekana ya kiume yasiyotoa matunda, Je haya yanikatishe nisipande tena mapapai? Jibu ni hapana. Natakiwa niendelee kupanda. Nikipanda nitapata yale yanayotoa matunda nami nitaendelea kula matunda.
Na Je. Nibadilishe biashara? Hapana do not give up. Usilegee, usikate tamaa, fanya kwa bidii. Utakapovuna utafurahi sana, Usife moyo na wala usilegee, fanya kwa wakati sahihi.
Fanya katika namna ambayo ukipanda utavuna. Nakila utakachokitia mkonono mwako kinatakiwa kiwe cha mafanikio. Fanya ufanikiwe.
Fanya kwa ujasiri.
Mtoto wa Mungu usikubali kuonekana makapi, haitapendeza. Tamani kuwa mwenye haki mbele za Mungu isiwe ulikuja duniani kwa hasara. Sisi tunatakiwa tusionekane kwamba ni makapi.
Methali4:6
Usimwache, naye atakuhifadhi;
Umpende, naye atakulinda.
Usimwache Yesu naye atakuhifadhi, umpende naye atakulinda.
Cha kufanya ni kuendelea kumpenda Yesu, wala tusiangalie watu. Tunapoendelea kumpenda na kuzidi kumpenda naye Yesu hutulinda na kutuhifadhi.
OMBA PAMOJA NAMI
Yeyote anayejua kuwa yeye ni kapi kwa namna moja au nyingine, wewe husomi neno la Mungu na wala hauna muda na Mungu hata wa kuomba omba sala hii pamoja nami naye Mungu ataonekana katika maisha yako:
Baba uliye juu mbinguni. Nalitukuza jina lako. Leo nimetambua maana ya kuwa makapi mbele zako. Naomba unisamehe kwa jina la Yesu. Nipe neema yako niwe karibu nawe, nikisoma neno lako na kuomba.
Niwe balozi mwema katika ufalme wako Mungu. Niwe mtu mwema kwa wengine. Nisiwe wa mizaha wala nisiketi katika baraza la wasio haki.
Ninaomba ujasiri, bidii na kutokukata tamaa.
Niwezeshe kusimamia maono ya maisha yangu. Nikufurahishe wewe Mungu wangu, na Yesu kristo, nami nikifurahi pia.
Nashukuru Baba yangu kwa yote. Katika jina la Yesu Kristo, Amina.
Laisser un commentaire